Mwelekezi wa filamu Souleymane Cissé afariki

Kifo chake kilijiri siku moja kabla ya safari ya kuelekea Burkina Faso kwa ajili ya Tamasha la filamu la Afrika.

Marion Bosire
2 Min Read
Souleymane Cissé

Souleymane Cissé, ambaye ni mwelekezi stadi wa filamu wa asili ya Mali amefariki akiwa na umri wa miaka 84. Binti yake ndiye alifichua hilo akielezea kwamba alifariki Jumatano katika jiji kuu Bamako.

“Baba alifariki leo huko Bamako. Sote tumeshtuka. Alijitolea maisha yake yote kwa nchi yake, kwa sinema na kwa sanaa.” aliandika Mariam Cisse.

Cissé alishinda tuzo ya waamuzi katika tamasha la filamu la Cannes mwaka 1987 kutokana na kazi yake kwa jina “Yeelen” inayomaanisha mwangaza ambayo inaangazia mashujaa wa Bambara magharibi mwa Afrika.

Mwaka 2023, waandalizi wa tamasha na tuzo za Cannes walimtambua tena kwa tuzo ya Carrosse d’Or, ambayo hutolewa kwa waelekezi ambao wameweka historia kwa ujasiri wao, viwango vyao na ustadi katika kuandaa maigizo.

Cissé hata hivyo aliibiwa tuzo hiyo kutoka nyumbani kwake mwaka 2024 kabla ya kupatikana tena.

Mwelekezi mwingine wa Mali Boubacar Sidibe alisema kupitia Facebook leo kwamba tasnia ya filamu katika eneo la Sahel inaombolewa huku waziri wa utamaduni nchini Mali Mamou Daffe akilalamikia kifo cha “mnara wa filamu Afrika”.

Cissé ni mmoja wa waandaaji filamu wawili ambao wamewahi kushinda mara mbili, tuzo ya kifahari ya wanaopenda Afrika ya Burkina Faso almaarufu Panafrican Film and Television Festival (FESPACO).

Alitarajiwa kusafiri leo kuelekea jiji kuu la Burkina Faso, Ouagadougou kuongoza kundi la waamuzi wa kitengo cha filamu za matukio halisi katika awamu ya 29 ya tamasha la Panafrican Film and Television Festival kuanzia Februari 22, 2025.

Share This Article