Rais wa kikao cha 79 cha Baraza la Umoja wa Mataifa (UNGA) Philemon Yang, atafanya ziara ya siku nne hapa nchini kuanzia Februari 18 hadi Februari 22, 2025.
Kulingana na taarifa kutoka kwa Waziri mwenye Mamlaka Makuu aliyepia Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, ziara hiyo inalenga kuimarisha jukumu la kenya katika maswala ya diplomasia duniani na uhusiano baina yake na Umoja wa Mataifa.
Wakati wa ziara yake, Yang atafanya mikutano ya ngazi za juu, akitarajiwa kukutana na Rais William Ruto, waziri mwenye Mamlaka Makuu Musalia Mudavadi, pamoja na maafisa wengine wakuu wa serikali.
Majadiliano hayo yataangazia kuimarishwa kwa ushirikiano baina ya Kenya na umoja wa mataifa.
“Rais huyo wa Baraza la Umoja wa Mataifa, atafafanua ruwaza yake wakati wa kipindi chake hususan kuhusu usalama na amani, maendeleo endelevu, ufadhi wa miradi ya maendeleo na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa,” ilisema taarifa hiyo.
Yang pia anatarajiwa kutoa hotuba ya umma pamoja na kukutana na baadhi ya waakilishi wa mataifa wanachama wa Umoja wa Mataifa humu nchini na wadau wengine muhimu wa sekta za kibinafsi, elimu na uvumbuzi.
Aidha Rais huyo atazuru maeneo ya bustani Jijini Nairobi na mbuga za wanyama.