Rushwa yamrusha kiongozi wa mashtaka matatani Kilgoris

Martin Mwanje
1 Min Read
Japheth Ouko Mayore Isaboke - Kiongozi Mkuu wa Mashtaka eneo la Kilgoris

Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) imemkamata Japheth Ouko Mayore Isaboke, Kiongozi Mkuu wa Mashtaka anayesimamia Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ya Kilgoris kwa tuhuma za kuitisha hongo.

Isaboke anadaiwa kuitisha hongo ya shilingi 50,000 kutoka kwa mfanyabiashara mmoja ili kesi dhidi ya mfanyabiashara huyo iharakishwe.

Baada ya mazungumzo kati yao, fedha hizo zilipunguzwa hadi 40,000.

Hata hivyo, mfanyabiashara huyo alikataa kulipa rushwa hiyo na badala yake kuripoti suala hilo kwa EACC.

Tume ilifanya operesheni iliyosababisha kukamatwa kwa kiongozi huyo wa mashtaka jana Jumapili wakati akipokea sehemu ya hongo hiyo yenye kima cha shilingi 20,000.

Mshukiwa alizuiliwa katika kituo cha polisi cha  Kisii na kisha kuachiliwa kwa dhamana ya shilingi 30,000 pesa taslimu akisubiri uchunguzi kukamilika.

TAGGED:
Share This Article