Kenya yaimarisha uchunguzi wa Mpox, Marburg na Ebola mipakani

Tom Mathinji
2 Min Read

Huku taifa hili likikumbwa na tisho la maambukizi ya Ebola, Mpox na Marburg hususan kutoka nchi jirani, Wizara ya Afya imechukua jukumu la kuimarisha uchunguzi mipakani na maeneo yote ya kuingia hapa nchini.

Katibu katika wizara ya afya ya umma Mary Muthoni, amesema uchunguzi wa mpakani ni muhmu sana huku uhamasishaji wa umma ukipewa kipaumbele katika kuzuia ueneaji wa maambukizi na hivyo kulinda afya ya umma.

Muthoni  aliyasema hayo leo Ijumaa alipozuru uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), kushauriana na kamati ya mpakani kuhusu uimarishaji uchunguzi wa magonjwa hayo na pia kuyakabili.

Katika ziara hiyo, Muthoni alitangaza kuwa sehemu ya Terminal 1A iliyo kwenye mlango wa 16 katika uwanja huo, utatumiwa na wasafiri wanaoingia hapa nchini kutoka Uganda na Tanzania, ambako magonjwa ya Ebola na Marburg yameripotiwa.

“Kenya inaendelea kulinda afya ya umma kupitia uchunguzi na kuwa tayari kwa dharura. Kwa kushirikiana na washirika wa kimataifa, tunaimarisha uwezo wetu wa kutambua na kushughulikia magonjwa yanayozuka mpakani,” alisema Muthoni.

Katika ziara hiyo kwenye uwanja wa JKIA, katibu Muthoni alikuwa ameandamana na mwakilishi wa Shrika la Afya Duniani(WHO) hapa nchini Dkt. Abdourahmane Diallo na afisa mkuu wa shirika la kimataifa la uhamiaji (IOM) Basnet Mukunda.

WHO na IOM zilielezea kujitolea kwao kusaidia Kenya kuimarisha juhudi zake za kukabiliana na dharura zinazochipuza za afya.

Share This Article