Afrika inahitaji shirika lake la kukadiria mikopo, asema Rais Ruto

Martin Mwanje
2 Min Read
Rais William Ruto wa Kenya

Kuna haja ya kubuni shirika la kukadiria mikopo kwa mataifa ya bara la Afrika kwa sababu mashirika ya kimataifa yaliyopo kwa sasa yanatumia dhana zilizopitwa na wakati na mifumo yenye upendeleo.

Rais William Ruto ameyatuhumu mashirika hayo kwa kuchora taswira isiyokuwa na usawa ya bara hilo, hali ambayo imesababisha viwango vilivyopotoshwa kutumiwa katika utoaji mikopo, hatari zilizotiliwa chumvi, na gharama za juu zaidi zisizokuwa na msingi za kuomba mikopo.

Ni kwa misingi hiyo ambapo Rais Ruto amesisitiza umuhimu wa kubuniwa kwa shirika la kukadiria mikopo barani Afrika.

Amesema shirika hilo, kwa kutumia data za kuaminika, litaakisi kwa usahihi ukweli wa bara la Afrika na kwa kufanya hivyo kutoa fedha zinazohitajika mno kufadhili mipango ya maendeleo barani humo.
“Ni wakati wa Afrika kutumia kipimo sahihi, kile kinachoakisi uzito wake wa kweli. Shirika la kukadiria mikopo la Afrika litafanya tu hilo,” alisema kiongozi wa taifa.

Kulingana naye, mashirika ya kimataifa ya kutoa mikopo yamekuwa mwiba kwa Afrika kwa kuikosea heshima na kuhujumu malengo yake ya maendeleo kimakusudi.

Rais Ruto aliyasema hayo leo Ijumaa asubuhi wakati wa kongamano la Umoja wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Wengine waliozungumza wakati wa kongamano hilo ni Marais Taye Atske Selassie (Ethiopia), Hakainde Hichilema (Zambia) na Abdelmadjid Tebboune (Algeria).

Ruto yuko nchini Ethiopia kuhudhuria Kikao cha Kawaida cha 38 cha Baraza la Wakuu wa Nchi na Serikali wa AU.

Share This Article