Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula amewaongoza wabunge katika kumtakia Raila Odinga kila la heri katika azma yake ya kugombea wadhifa wa uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Wetang’ula aliyasema hayo leo Jumatano wakati akishangiliwa na wabunge kutoka mirengo yote ya Kenya Kwanza na Azimio na angalau kupooza machungu ya Azimio hata kama ni kwa muda mfupi tu.
Machungu hayo yalitokana na uamuzi wa Wetang’ula kuwa Kenya Kwanza ndio muungano ulio na wabunge wengi katika Bunge la Taifa.
Raila, ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, analenga kumrithi Moussa Faki ambaye anaondoka baada ya kuhudumu kwa mihula miwili.
Faki alimshinda Mkenya mwengine, Waziri wa zamani wa Elimu Balozi Amina Mohamed kabla ya kuchaguliwa kwenye wadhifa huo.
Raila anatumai mmoja wa wapinzani wake, ama Mahamoud Ali Youssouf ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti au Richard Randriamandrato ambaye ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Madagascar, hatakuwa sababu ya yeye kukosa wadhifa huo.
Marais wa nchi za bara la Afrika watapiga kura Jumamosi hii, Februari 15, 2025, kumchagua mmoja kati ya watatu hao kumrithi Faki.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Musalia Mudavadi ameapa kufanya kampeni kali za lala salama kumnadi Raila kabla ya kura za kumwamua mshindi kupigwa.
Mudavadi tayari ametua jijini Addis Ababa kwa wajibu huo.
Wengi hasa wanakisia kwamba Raila atakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa mgombea wa Djibouti.
Hata hivyo, Raila ambaye amekuwa akitembelea mataifa mbalimbali ya Afrika kuwinda kura, ameelezea imani kuwa atashinda wadhifa huo.