Kenya inahitaji zaidi ya shilingi bilioni moja kuweka mikakati itakayosaidia jamii zinazokabiliwa na uhaba wa chakula katika maeneo kame (ASALs) hapa nchini.
Huku ikiwasilisha taarifa yake kwa naibu Rais Prof. Kithure Kindiki, kamati tekelezi ya kitaifa ya kukabiliana na majanga (NDRSC), ilidokeza kuwa watu miliono 1.8 kwa sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula katika kaunti tano hapa nchini.
Kamati hiyo pia ilimfahamisha naibu huyo wa Rais kuhusu athari zinazotarajiwa katika msimu ujao wa mvua za masika za mwezi Machi hadi Mei (MAM).
Mwakilishi wa kamati ndogo ya mawasiliano ambaye pia ni Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji nchini KBC Agnes Kalekye, alisema kamati hiyo inafanya tathmini ya kina kuhusu ukame na kupigia kurunzi hatua zinazochukuliwa na wizara husika kukabiliana na athari za ukame, ikiwa ni pamoja na usambazaji chakula kwa zaidi ya familia 200,000 katika maeneo yaliyotengwa.
Mwenyekiti wa kamati hiyo Dkt. Peter Ndegwa, pia alielezea wasiwasi kuhusu hatua ya Marekani kusitisha misaada ya kibinadamu.
Hayo yalijiri huku halmashauri ya kitaifa ya kukabiliana na ukame, ikitoa onyo kuhusu ikame katika kaunti 18, wasiwasi ukitanda kuhusu uwezekano wa mvua za masika kufeli.
Utabiri wa hali ya hewa unaashiria kuwa kutakuwa na mvua ya wastani kati ya mwezi Machi, Aprili na Mei, katika maeneo kadhaa hapa nchini.