Seneta Orwoba kukosa vikao vya bunge kwa miezi mitatu

Martin Mwanje
1 Min Read
Gloria Orwoba - Seneta mteule

Marufuku iliyotolewa awali na Bunge la Seneti dhidi ya Seneta mteule Gloria Orwoba imeanza kutekelezwa leo Jumatano. 

Tangazo la Seneta Orwoba kuanza kutumikia marufuku hiyo ya takriban miezi mitatu limetolewa na Naibu Spika Kathuri Murungi wakati wa kikao cha leo Jumatano asubuhi.

Bunge la Seneti mwezi Septemba mwaka jana  kwa kauli moja lilipitisha hoja ya kumfungia nje Seneta huyo kwa ukaidi.

Hii ni baada ya Orwoba kutoa madai ya ufisadi na dhuluma za kunyanyaswa kimapenzi dhidi ya Maseneta wenzake.

Alipotakiwa kuyathibitisha, alishindwa kufanya hivyo na pia akadinda kufika mbele ya kamati ya nidhamu ya bunge hilo ili kujitetea.

“Naomba msamaha kwa bunge hili na yeyote ambaye nilimkosea katika kuwasilisha hoja yangu. Sikukusudia,” alisema Orwoba kabla ya kufunganya virago na kuondoka katika ukumbi wa Bunge la Seneti.

Seneta Orwoba alielekea mahakamani kupinga marufuku dhidi yake, kesi ambayo ilitupiliwa mbali na mahakama kukubaliana na uamuzi wa Seneti.

Aanatarajiwa kutumikia marufuku hiyo hadi Mei 1, 2025.

Seneta huyo hatalipwa marupurupu ya vikao wakati wa marufuku hiyo.

 

 

Share This Article