Rais William Ruto ametoa wito kwa jamii ya wafanyabiashara kutoka Saudi Arabia kutafuta fursa za uwekezaji humu nchini.
Ruto amesema serikali yake imeweka mpangokazi madhubuti kwa kusudi la kuwezesha ushiriano wa sekta ya umma na ile ya kibinafsi ili kuvutia uwekezaji.
Ameongeza kuwa serikali iko tayari kuchukua hatua zadi za kuinadi Kenya kama kituo cha uwekezaji.
“Tayari tuna mpangokazi ambao ni wezeshi kwa ajili ya uwekezaji wa sekta ya umma na kibinafsi ili kuchochea uwekezaji katika sekta hizo mbili,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa nchi aliyasema hayo katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne, wakati wa mkutano na uongozi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Saudi Arabia na jumuiya yake ya biashara.
Ruto aliwahakikishia wawekezaji kuwa Kenya ni thabiti na nchi kubwa kiuchumi inayopatikana eneo zuri kijiografia.
“Hamtafanya tu kazi na nchi kubwa kiuchumi, lakini pia itahudumu kama lango lenu kwa bara la Afrika,” aliongeza Rais.
Ujumbe wa Saudia ulijumuisha Balozi wa nchi hiyo humu nchini Khalid Alsalman, Mwenyekiti wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Saudia Bani Huwayz Hassan Mujib na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Alorainan Waleed Hamad.
Mujib akielezea kuwa Saudi Arabia ina fursa za ajira 50,000 za wauguzi.
“Tuna tajiriba nzuri na chanya na wauguzi kutoka Kenya,” aliungama Mujib.
Waziri wa Biashara wa Kenya Lee Kinyanjui aliishi jumuiya ya biashara ya Saudia kutumia ukaribu na uhusiano thabiti uliopo baina ya nchi hizo mbili kuwekeza humu nchini.