Rais wa Marekani Donald Trump ameamuru kutozwa ushuru wa forodha wa asimia 25 kwa chuma na alumini zote zinazoingia nchini humo katika upanuzi mkubwa wa vikwazo vya biashara vilivyopo.
Ushuru huo, ambao utaongeza gharama za kuagiza bidhaa hizo nchini Marekani, unakuja licha ya onyo la kulipiza kisasi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa nchini Canada – msambazaji mkubwa zaidi wa bidhaa hizo nchini Marekani – pamoja na nchi zingine.
Biashara za Marekani zinazotegemea uagizaji bidhaa hizo pia zimeibua wasiwasi, lakini Trump amesema mipango yake itaongeza uzalishaji wa ndani.
Alionya kuwa hakutakuwa na ubaguzi, akisema “anarahisisha” sheria, ambazo zimepangwa kuanza kutumika Machi 4.
“Hili ni jambo kubwa, mwanzo wa kuifanya Marekani kuwa tajiri tena,” Trump alisema.
“Taifa letu linahitaji chuma na alumini kutengenezwa Marekani, sio katika nchi za kigeni,” aliongeza.
Alipoulizwa kama ushuru unaweza kuongeza bei kwa watumiaji, Rais huyo alijibu: “Hatimaye itakuwa nafuu.”
“Ni wakati wa viwanda vyetu vikubwa kurejea Marekani…hii ni ya kwanza kati ya nyingi,” aliongeza, akipendekeza ushuru mwingine unaweza kuwekwa kwa dawa na chipu za kompyuta.
Marekani ndiyo nchi inayoongoza duniani kuagiza chuma, huku Canada, Brazil na Mexico zikiwa wasambazaji wake wakubwa.