Mwenyekiti wa jopo la kuwateua Makamishna na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Dkt. Nelson Makanda amewahimiza wanachama wa jopo hilo kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu, bidii na usawa.
Dkt. Makanda aliyasema hayo jana Jumatatu wakati wa ufunguzi rasmi wa mkutano wa siku tano unaojumuisha wadau wa uchaguzi mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.
Huku zikiwa zimesalia siku tano tu kabla ya kukamilika kwa muda wa kutuma maombi kwa nyadhifa hizo, Dkt. Makanda alisema mfumo utakaotumiwa na jopo hilo kuwachagua Makamishna na Mwenyekiti wa IEBC, utabainisha ikiwa uchaguzi mkuu ujao utafaulu au utakumbwa na changamoto.
“Tunapaswa kutekeleza jukumu hili kwa uadilifu wa hali ya juu, bidii na usawa,” alihimiza Dkt. Makanda.
Kulingana na mwenyekiti huyo, taifa hili linahitaji IEBC ambayo ni ya kuaminika, itakayokumbatia utaalam wa hali ya juu na ambayo itasalia thabiti licha ya shinikizo za kisiasa.
Kwa upande wake, Naibu Mwenyekiti wa tume hiyo Lindah Kiome alisema atajizatiti kuhakikisha mchakato wa kuwateua makamshna na mwenyekiti wa IEBC unakuwa jumuishi na utakaozingatia sheria na maadili.
“Mimi kama Naibu Mwenyekiti, ninajitolea kumuunga mkono mwenyekiti na wanachama wa jopo hili, kuhakikisha tunazingatia utaalam wa hali ya juu, sheria na maadili,” aliahidi Kiome.