Viongozi wa eneo la kaskazini mashariki mwa nchi wamewashutumu kinara wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya kutokana na hatua yao ya kupinga kuondolewa kwa hitaji la kuwafanyia wakazi wa eneo hilo ukaguzi kabla ya kupatiwa vitambulisho vya kitaifa.
Wakiwahutubia wanahabari leo Jumanne katika majengo ya bunge, viongozi hao, wakiongozwa na wabunge Farah Maalim (Dadaab) na Adan Keynan (Eldas) wamesema ni haki ya kila Mkenya kupata vitambulisho vya kitaifa.
“Ni haki ya kikatiba kwa kila Mkenya kupata kitambulisho cha kitaifa na pasipoti,” walisisitiza viongozi hao.
Katika kupinga hatua hiyo, Natembeya ameonya kuwa hatua ya kuwapa wakazi wa kaskazini mashariki vitambulisho bila kuwafanyia ukaguzi itakuwa hatari kwa taifa hili.
“Jambo hili lina maana kubwa ya usalama, hili silo jambo la kufanya kwa namna yoyote kwani itafikia hatua kwamba hata MCA atachaguliwa kutoka kwa makundi yaliyopigwa marufuku nchini,” Natembeya amenukuliwa akionya.
Msimamo sawia umeripotiwa kuchukuliwa na Kalonzo.
Wakati wa ziara yake katika eneo la kaskazini mashariki mwa nchi siku chache zilizopita, Rais William Ruto aliwaondolea wakazi wa eneo hilo hitaji la kufanyiwa ukaguzi kabla ya kupewa vitambulisho vya kitaifa.
Katika kutia saini amri ya kuondoa hitaji hilo, Rais Ruto alilitaja kuwa la kiubaguzi.
“Raia wenzetu kutoka kaskazini mwa Kenya hawatahitaji kamwe kupitia mateso yanayowakosea heshima ya kufanyiwa ukaguzi zaidi na kubaguliwa kikabila kabla ya kukabidhiwa nyaraka za utambulisho wa kitaifa,” alisema Ruto alipotia saini amri hiyo katika uwanja wa Orahey mjini Wajir Jumatano wiki iliyopita.
Rais alisema kila Mkenya yuko sawa mbele ya sheria na hafai kubaguliwa kwa misingi ya rangi, kabila au eneo analotoka.
Aliongeza kuwa uamuzi huo uliafikiwa kufuatia malalamiko mengi hasa kutoka kwa jamii ya Waisilamu yaliyowasilishwa kwa ofisi yake, bunge na taasisi zingine za serikali.