Tume ya Maadili na Kupambanana na Ufisadi (EACC) imeanzisha mpango mahususi wa kufanya ukaguzi wa shughuli za Huduma ya Taifa ya Polisi (NPS).
EACC imeanzisha mpango huo utakaotathmini shughuli zote, mikakati na sera ya polisi ili kubaini mapungufu yaliyopo NPS yanayochangia ufisadi.
Mwenyekiti wa EACC, Dkt .David Oginde, akiandamana na Afisa Mkuu Mtendaji Abdi Mohamud, akisema mbinu hizo zilizoanzishwa zitahakikisha uaminifu, uwajibikaji na huduma bora.
Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amesema kama NPS, wanakumbatia ukaguzi huo ambao utachangia idara ya polisi kutoa huduma bora.
Wote hao walizungumza wakati wa uzinduzi wa ukaguzi wa kina wa mifumo, sera, taratibu na utendakazi wa NPS uliofanyika katika Chuo cha Taifa cha Polisi cha Embakasi jana Jumatatu.
Idara ya Polisi imeorodheshwa kuwa miongoni mwa taasisi fisadi zaidi nchini, huku polisi wa trafiki wakiripotiwa kuchangia uvundo huo kwa kiwango kikubwa.
EACC imeapa kufanya kila iwezalo kukabiliana na jinamizi la ufisadi ambalo limeachangia kukwama kwa miradi ya serikali na Wakenya kukosa huduma muhimu kama vile matibabu kutokana na ufisadi na ubadhirifu wa rasilimali za umma.