Rais William Ruto ameahidi kuwa nchi hii imekusudia kuimarisha ushirikiano wa pande mbili na pande nyingi na mataifa yote kwa lengo la kuhakikisha watu wote duniani wananufaika na matokeo bora.
“Tutapigania na kupanua uhusiano wa kidiplomasia, kukuza mashauriano ya kimkakati na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuboresha zaidi mafanikio yetu ya pamoja,” alisema Rais Ruto alipowahutubia Mablozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa katika Ikulu ya Nairobi leo Jumatatu.
Amesema hotuba yake ya Kidiplomasia ya Mwaka Mpya kwao ni ishara tosha ya dira iliyochukua Kenya kuhusiana na masuala ya kidiplomasia, ambayo haiangazii tu maslahi ya taifa bali pia inaimarisha ushirikiano, kukuza heshima na kuhamasisha malengo ya pamoja.
“Tangu uhuru, tumepanua uwepo wetu wa kidiplomasia kutoka balozi sita hadi 70. Tunaendelea kutoa kipaumbele kwa utangamano wa kikanda, uhusiano baina ya mataifa ya Afrika, diplomasia ya kiuchumi, na amani na usalama wa dunia.”

Kama mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais Ruto amesema Kenya imedhamiria kuhakikisha umoja huo unaafikia malengo yake kwa kutumia mafanikio yaliyoafikiwa siku zilizopita.
Rais pia amesisitiza haja ya kuufanyia mabadiliko Umoja wa Afrika (AU) ili kuuwezesha kukabiliana vilivyo na changamoto zinazoibuka barani Afrika kama vile utatuzi wa migogoro, maendeleo ya kiuchumi na maongozi bora.
“Kenya pia imejivunia kumteua Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kugombea wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, AUC. Ugombea wake unaakisi maono mapana ya Kenya ya kuimarisha taasisi hiyo ya Afrika ili kutoa huduma bora kwa watu wa bara hili.”

Maombi ya kumwombea Raila kwa wadhifa huo yalifanyika leo Jumatatu katika ukumbi wa Bomas kabla ya shughuli ya kupiga kura kufanyika mwishoni mwa wiki hii kumtafuta mrithi wa Moussa Faki ambaye muhula wake wa kuhudumu unaelekea kumalizika.