Wanafunzi wapatao 17 wanaripotiwa kuangamia katika mkasa wa moto uliozuka kwenye shule moja ya kiisilamu katika jimbo la Zamfara nchini Nigeria.
Moto huo katika shule ya Almajiri huko Kauran Namoda, uliacha wanafunzi wengine wengi na majeraha na iligharimu muda wa saa kama tatu kuuzima.
Wahudumu wa nyakati za dharura pamoja na wakazi wa eneo la karibu na shule hiyo walijibidiisha kuzima moto huo na kusaidia wanafunzi ambao walipelekwa kwenye taasisi za afya zilizo karibu kwa matibabu.
Maafisa wameanzisha uchunguzi kufahamu chanzo cha moto huo huku serikali ya jimbo la Zamfara ikiahidi kusaidia waathiriwa huku ikichunguza upya mikakati ya usalama katika taasisi za elimu.
Tukio hilo ni la Jumanne februari 4, 2025 usiku.
Walioshuhudia wanasema moto huo ulisambaa haraka shuleni humo na kuteketeza sehemu kubwa ya majengo na kusababisha wanafunzi wengi kukwama ndani ya majengo fulani.
Wahudumu wa afya walipelekwa katika eneo la tukio kutoa huduma ya kwanza huku walioshuhudia wakisema hali ilikuwa ya wasiwasi kila mmoja akionekana kuchanganyikiwa.