Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ndiye mshindi wa mwaka huu wa tuzo ya The Global Goalkeeper. Alipokezwa tuzo hiyo rasmi leo Jumanne Februari 4, 2025 katika hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam.
Tuzo za Global Goalkeepers ni mpango ulioanzishwa na wakfu wa Bill and Melinda Gates mwaka 2017 kwa lengo la kukutanisha viongozi kutoka kote ulimwenguni ili kuharakisha mchakato wa kuafikia malengo ya maendeleo endelevu.
Hafla kuu ya tuzo hizo huwa kongamano la kila mwaka la viongozi ambao wamewahi kupokea tuzo hiyo ambalo huandaliwa wakati wa wiki ya malengo ya dunia na kongamano kuu la umoja wa mataifa yaani UN General Assembly.
Tuzo hiyo hutolewa kwa watu wa kipekee ambao wanaendesha maendeleo katika jamii zao na nchi zao.
Wale ambao wamewahi kuhudhuria kongamano la tuzo hizo ni pamoja na Rais wa 44 wa Marekani Barack Obama, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Rais wa Brazil Luiz Inácio Lula da Silva, Amina J. Mohammed, Erna Solberg, Malala Yousafzai na Trevor Noah.
Washindi wa awali wa tuzo hiyo ya Global Goalkeeper ni pamoja na Yusra Mardini, Amika George, Ria Sharma na Nadia Murad.