Wizara ya Afya nchini imekumbusha wakenya wote kwamba marufuku ya Shisha bado ipo na inatekelezwa kikamilifu.
Katika taarifa, Katibu wa Afya ya Umma Mary Muthoni alisema kulingana na marufuku hiyo ya mwaka 2017 chini ya sheria za Afya ya Umma, hakuna anayeruhusiwa kutengeneza, kuagiza, kuuza na kutumia Shisha humu nchini.
Uvutaji Shisha umehusishwa na hatari mbali mbali za kiafya kama vile magonjwa na pumu, ya moyo na kujiweka katika hatari ya kuingiwa na kemikali mbaya.
Hata ingawa marufuku hiyo ilipingwa mwaka 2018 katika mahakama kuu, mahakama ya upeo iliidumisha mwaka 2024 na kutanguliza afya ya umma badala ya maslahi ya kibiashara.
Wizara hiyo kwa ushirikiano na idara nyingine za serikali, inaendelea kutekeleza sheria hiyo ya kupiga marufuku Shisha huku ikiwataka maafisa wa utekelezaji sheria kufanya msako na kukamata wahusika.
Wakenya wanahimizwa kutanguliza afya yao na ya wapendwa wao huku wakikumbushwa kwamba kinga ni bora kuliko tiba.