Maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai DCI, wanamtafuta mshukiwa wa ulanguzi wa bidhaa za wanyamapori, ambaye amesusia vikao vya mahakama.
Kupitia mtandao wa X, idara ya DCI imesema Alfred Mbugua Gicheha, alikamatwa Mei 24, 2023 katika eneo la Sipili kaunti ya Laikipia akiwa na pembe 23 za wanyamapori zenye thamani ya shilingi 11,050,000.
Idara hiyo iliongeza kuwa Gicheha alifunguliwa mashtaka katika mahakama ya JKIA Mei 27,2023 na aliachiliwa kwa dhamana ya shilingi milioni tatu.
Baada ya mashahidi wote kutoa ushahidi wao, mshukiwa huyo alipatikana na hatia ya kujihusisha na bidhaa za wanyamapori bila kibali.
Hata hivyo tangu mwezi Disemba mwaka 2023, amesusia vikao vya mahakama, hatua iliyomlazimu hakimu wa mahakama hiyo kutoa kibali cha kukamatwa kwa mshukiwa huyo.
Maafisa wa polisi wametoa wito kwa yeyote aliye na habari kumhusu kuripoti kwa idara ya DCI, au kituo cha polisi kilicho karibu.