Miili ya wanajeshi kadhaa ilipatikana imetapakaa mjini Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), siku kadhaa baada ya makabiliano makali kati ya wanajeshi wa serikali na kundi la waasi wa M23 linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda.
Makabiliano baina ya wanajeshi na waasi wa M23 yamekuwa yakiendelea mjini Goma tangu Januari 26 mwaka huu.
Hali hiyo imewalazimu wakazi wengi kutoroka makwao huku wakikabiliwa na ukosefu wa maji na kukatika kwa umeme.
Wakazi hao wanatoa wito wa kurejeshwa kwa hali ya usalama katika mji huo mara moja.
Licha ya M23 kuwataka wafanyabiashara kurejelea shughuli zao, maeneo mengi yangali yamefungwa yamkini kutokana na hofu ya kutofahamu kitakachojiri baadaye.
Kulingana na Umoja wa Mataifa, M23 inaungwa mkono na takriban maafisa wa polisi 4,000 wa Rwanda.