Patti Smith mwanamuziki wa Marekani alizirai akiendelea kutumbuiza jukwaani nchini Brazil, dakika 30 tu baada ya kuanza kuimba.
Mwimbaji huyo wa umri wa miaka 78 alikuwa akitumbuiza katika ukumbi wa Cultura Artística mjini Sao Paulo kwa ushirikiano na kampuni ya Soundwalk Collective group ya Berlin Ujerumani.
Inaripotiwa kwamba tatizo hilo la kiafya lilimfika Patti akisoma ujumbe fulani kuhusu mabadiliko ya tabianchi.
Patti aliondolewa jukwaani na kurejea baadaye kidogo akitumia kiti cha magurudumu ambapo aliomba radhi wahudhuriaji akielezea kwamba daktari wake alimkataza asiendelee kuimba.
“Kwa bahati mbaya nimeugua na daktari amesema siwezi kuendelea. Hivyo tutalazimika kutafura namna. Na ninajihisi vibaya.” alisema Patti.
Kampuni ya Soundwalk nayo ilitoa taarifa kupitia akaunti yake ya Instagram ambapo ilielezea kwamba mwanamuziki huyo alikuwa ameugua maumivu ya kichwa kwa siku kadhaa na alipokuwa jukwaani akahisi kusunzi.
Iliahidi kwamba mwanamuziki huyo atarejelea tumbuizo lake kesho iwapo hali yake ya kiafya itaimarika huku ikisisitiza kwamba anahudumiwa na madaktari bora kwa njia ya upendo.