Mwanamume mmoja kati ya wanne waliotekwa nyara katika eneo la Mlolongo, kaunti ya Machakos mwezi Disemba mwaka jana amepatikana akiwa ameuawa.
Mwili wa Justus Musyimi ulipatikana leo Alhamisi katika chumba cha kuhifadhi maiti ya City jijini Nairobi.
Musyimi, Martin Mwau, Kalani Muema na Stephen Kavingo walitekwa nyara na watu wasiojulikana mwezi Disemba mwaka jana.
Leo Alhamisi, Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) Amin Mohamed walikuwa mahakamani kuelezea hatima ya wanne hao.
Ni wakati huo ambapo familia ya Musyimi ilifahamishwa kuwa miili miwili imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha City.
Jamaa waliokuwa wakihudhuria kesi mahakamani walikimbia hadi chumba hicho na kubaini kuwa mmoja wa miili hiyo ulikuwa wa mwanao Justus Musyimi.
Mwili mwingine bado haujatambuliwa.
Kanja amekanusha kuhusika kwa maafisa wa polisi katika visa vinavyoongezeka vya utekaji nyara na anasema uchunguzi kwa lengo la kuwakamata wahusika bado unaendelea.