Willy Paul na Bahati kuzindua kazi za pamoja kesho

Wawili hao walirejelea urafiki wao wa awali Novemba mwaka jana na sasa wameshirikiana katika nyimbo mbili.

Marion Bosire
2 Min Read

Wanamuziki Willy Paul na Bahati wote wa Kenya wanatarajiwa kuzindua nyimbo mpya ambazo wameshirikiana kesho, kulingana na tangazo kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii.

Willy alichapisha picha ambayo inaonyesha wawili hao wakishindana kwenye mchezo wa nguvu za mikono huku kibao cha mchezo wa chess kikiwa katikati yao.

“Wafalme wawili, nyimbo mbili. Balaa mara mbili. Nyimbo zote mbili zitatolewa kesho saa nne asubuhi.” aliandika Willy Paul huku akitania mashabiki akiwaambia wakanye wanamuziki wawapendao wasitoe nyimbo zao kwa sasa.

Aliendelea kusema kwamba waliamua kufanya kazi hizo kwa ajili ya tasnia ya muziki nchini Kenya ili irejelee uzuri wake wa awali.

Kulingana naye video za nyimbo hizo zilinakiliwa ughaibuni.

Mwezi Novemba mwaka 2024 wasanii hao, ambao waliwahi kuwa marafiki na kushirikiana kikazi wakiwa kwenye ulingo wa nyimbo za injili, walirejelea urafiki wao.

Willy Paul alianza kwa kumwomba Bahati na mkewe Diana msamaha kutokana na matamshi yake ya awali ambayo yalisababisha kutoelewana kati yao.

Msanii huyo aliwahi kusema kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi awali na Diana ambaye ni mke wa Bahati, usemi ambao alibatilisha na kuomba msamaha.

Baadaye tena alichapisha picha ya pamoja na Bahati akisema wametoka mbali, tangu wakati alimpa makazi hadi wakati Bahati alimshauri kuhusu maisha.

“Kuungana tena kuna maana kubwa sana kwangu ndugu yangu. Shetani nusura afanikiwe lakini kama kawaida Mungu huwa hatua mbele. Sina lingine ila upendo tu kwako ndugu.” aliandika Willy Paul chini ya picha hiyo ya pamoja na Bahati.

Share This Article