Brussels Airlines yafuta safari za ndege kuelekea Kinshasa, DRC

Martin Mwanje
1 Min Read

Shirika la ndege la Brussels Airlines limefuta safari zake za leo Jumatano kuelekea na kutoka mjini Kinshasa kufuatia vurugu katika mji huo mkuu wa Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC. 

Jana Jumanne, raia wa nchi hiyo walizua vurugu na kushambulia balozi za nchi mbalimbali kulalamikia mgogoro unaotokota mashariki mwa nchi hiyo.

Shirika la Brussels Airlines hufanya safari za kila siku za kwenda na kutoka Brussels-Kinshasa.

“Uamuzi wa kurejelea safari hizo utafanywa baada ya tathmini ya kina na angalifu ya hali ya usalama,” lilisema shirika hilo la Ubelgiji katika taarifa.

Waandamanaji wameghadhibikia hatua ya jumuiya ya kimataifa kutochukua hatua kusitisha mgogoro mashariki mwa DRC.

Jana Jumane, walielekeza hamaki zao kwa balozi za Rwanda, Kenya, Uganda, Ufaransa, Ubelgiji na Marekani.

Supamaketi pia ziliporwa na rundo la matairi kuchomwa moto barabarani wakati wa maandamano yenye vurugu mjini Kinshasa.

Kenya, Ufaransa na Umoja wa Ulaya zimelaani kushambuliwa kwa balozi hizo.

Waandamanaji wanaituhumu Rwanda na Uganda kwa kuunga mkono waasi wa M23 ambao wamedai kuudhibiti mji wa Goma.

 

Share This Article