Maafisa wa polisi kutoka kituo cha polisi cha Kutus kaunti ya Kirinyaga, wamefanikiwa kumuokoa mtoto wa umri wa miezi 14 aliyekuwa ametekwa nyara.
Maurine Kariuko aliripotiwa kutoweka Januari 23,2025, akiwa mikononi mwa jamaa wa familia yake.
Kupitia ukurasa wa X, idara ya upelelezi wa makosa ya jinai DCI, ilisema mama wa mtoto huyo alikwenda kutengenezwa nywele na kumuacha mwanawe na jamaa wa familia. Aliporudi alipata wawili hao wametoweka.
Kulingana na DCI, maafisa wake walianzisha operesheni mara moja kumtafuta mtoto huyo.
Operesheni hiyo ilizaa matunda, baada ya jamaa kutiwa nguvuni katika eneo la Piai kaunti ya Kirinyaga akiwa na mtoto huyo.
Huku uchunguzi ukiendelea, Maurine ameunganishwa na familia yake.