Makosa aliyoshtakiwa kwayo Besigye

Marion Bosire
2 Min Read
kiongozi wa upinzani wa Uganda Kizza Besigye.

Kanali mstaafu wa Uganda Kiiza Besigye na mshtakiwa mwenza Haji Obeid Lutale, wameshtakiwa rasmi kwa makosa kadhaa katika mahakama ya kijeshi ya Makindye.

Kulingana na hati ya mashtaka ambayo imesambazwa mitandaoni, makosa hayo yanatokana na matendo yanayochukuliwa kuwa ya kuhatarisha usalama wa kitaifa wa Uganda.

Upande wa mashtaka unasema kwamba kati ya Oktoba na Novemba 2024, Besigye, Lutale na washirika wengine waliandaa mikutano huko Geneva, Athens na Nairobi kwa lengo la kutafuta fedha za kufadhili utambuzi wa maeneo ya kijeshi nchini Uganda.

Matendo hayo yameorodheshwa kama makosa yanayohusiana na usalama chini ya sehemu ya 128 (1) ya sheria ya jeshi la Uganda nambari 330.

Wawili hao wanakabiliwa pia na makosa kadhaa ya kumiliki bunduki na risasi kinyume cha sheria.

Wanaripotiwa kupatikana na bastola aina ya 27KAL na nyingine aina ya HB 1014 1953 mnamo Novemba 16, 2024, katika makazi ya Riverside Apartments, jijini Nairobi.

Silaha hizo zinaruhusiwa kwa wanajeshi pekee nchini Uganda. Wanadaiwa pia kupatikana na risasi 8, hatua iliyozidisha uzito wa mashtaka dhidi yao.

Mahakama hiyo ya kijeshi haitatoa tarehe ya kusikilizwa kwa kesi ya wawili hao ambayo huenda ikavutia umma na vyombo vya habari.

Haya yanajiri saa chache tu baada ya mke wa Besigye kutangaza kwamba mume wake alikamatwa akiwa Nairobi na anazuiliwa nchini Uganda.

Share This Article