Mwakilishi wa taifa la Panama kwenye shindano la Miss Universe Italy Mora, amezungumza kuhusu kuondolewa kwake ghafla kwenye shindano hilo.
Alithibitisha kwamba hatua hiyo ni adhabu ya hatua yake ya kutoka kwenye chumba chake cha kulala bila idhini.
Mora amesikitishwa na uamuzi wa kumbandua kwenye shindano hilo akiutaja kuwa adhabu kali sana. Anasema alifahamishwa kuhusu hilo wakati alikuwa akijiandaa kuhudhuria hafla ya chajio.
“Ninakubali kosa la kutoka chumbani bila idhini lilitokea ila nilikwenda kupodolewa na kuchukua vitu vyangu.” alisema Mora akiongeza kwamba aliamini alifuata maagizo bila kufikiria athari zake.
Hata hivyo mrembo huyo anahisi kwamba suala hilo lingetatuliwa kupitia mazungumzo na yeye kupatiwa onyo.
Alikanusha madai yaliyosambazwa awali kwamba alizozana na mshindani mmoja na kwamba alikwenda kukutana na mpenzi wake punde baada ya kuwasili Mexico.
Awamu ya 73 ya shindano la urembo la Miss Universe inaandaliwa huko Mexico kati ya Novemba 14 na 16 huko Mexico, huku hafla ya kutuza washindi ikiandaliwa Novemba 17, 2024 katika ukumbi wa Arena CDMX.