Waziri Mkuu wa Japani Shigeru Ishiba leo Jumatatu ameapa kusalia madarakani licha ya hatua yake ya kuitisha uchaguzi wa ghafla kupata pigo.
Muungano wake wa vyama tawala ulishindwa kupata idadi kubwa ya viti kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2009.
Ishiba aliitisha uchaguzi wa jana Jumapili baada ya kuingia madarakani Oktoba 1.
Lakini wapiga kura waliokuwa na hamaki kutokana na kashfa ya uchangishaji fedha walikiadhibu chama chake cha Liberal Democratic (LDP), ambacho kimeiongoza Japani yamkini wakati wote tangu mwaka 1955.
Ishiba mwenye umri wa miaka 67 amesisitiza leo Jumatatu kuwa ataendelea kuhudumu akisema hataruhusu “ombwe la kisiasa” katika taifa hilo ambalo ni la nne kwa ukubwa kiuchumi duniani.
Amesema kigezo kikubwa zaidi cha uchaguz huo kilikuwa “mashaka, ukosefu wa uaminifu na hasira za watu” baada ya kashifa ya chama hicho ambayo ilisaidia kumuondoa madarakani mtangulizi wake Fumio Kishida.
“Nitatekeleza marekebisho muhimu juu ya suala la fedha na siasa,” Ishiba aliwaambia wanahabari.
Kulingana na utabiri wa shirika la habari la serikali la NHK na mashirika mengine, LDP na chama mshirika wake mdogo katika muungano unaotawala Komeito vilishindwa kupata viti 233 kama alivyokusudia Ishiba, ambavyo ndivyo viti vingi vinavyohitajika katika Baraza la Chini la Bunge lenye viti 456.
LDP ilishinda viti 191 ambavyo vilipungua kutoka viti 259 katika uchaguzi mkuu uliopita uliofanywa mwaka 2021 na Komeito kupata viti 24, kulingana na hesabu za NHK. Matokeo rasmi bado hayajachapishwa.