Chama cha ODM kimekanusha madai kuwa kinara wake Raila Odinga ameitisha mkutano wa wabunge wa chama hicho kuhusiana na hoja ya kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Baadhi ya vyombo vya habari vilidai Raila alipanga kukutana na wabunge hao leo Jumatatu kabla ya hoja ya kumbandua Gachagua kuwa mada itakayojadiliwa kwa mapana na marefu na kisha kupigiwa kura bungeni kesho Jumanne.
“Hakuna mkutano kama huo uliopangwa kufanywa leo,” kilisema chama hicho katika taarifa fupi.
Gachagua amepangiwa kufika bungeni kesho Jumanne kujitetea dhidi ya mashtaka 11 yaliyowasilishwa dhidi yake.
Anatuhumiwa kwa miongoni mwa mambo mengine kueneza ukabila na kujizoelea mali ya mabilioni ya pesa kwa kipindi kifupi alichohudumu kama Naibu Rais kwa njia za kutilia shaka.
Hoja ya kumbandua Gachagua imewasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.