Uteuzi wa Kanja waidhinishwa na bunge la Seneti

Marion Bosire
2 Min Read

Bunge la Seneti limeidhinisha uteuzi wa Douglas Kanja kuwa Inspekta Jenerali wa polisi kufuatia pendekezo la kamati ya pamoja ya bunge la taifa na la seneti iliyomsaili wiki jana.

Baada ya kumsaili kamati ya bunge la taifa kuhusu usimamizi na usalama wa ndani na ile ya Seneti kuhusu usalama wa taifa zilikubali kwamba Kanja anatosha kuhudumu katika wadhifa huo.

Sheria za bunge la taifa na za bunge la Seneti zinaelekeza kwamba uteuzi wa Inspekta Jenerali uidhinishwe na mabunge hayo mawili.

Maseneta walimsifia Kanja wakionyesha imani kwamba atatekeleza wajibu wake ipasavyo huku wakimpa changamoto ya kutekeleza mabadiliko katika huduma ya taifa ya polisi.

Seneta wa kaunti ya Nyamira Eric Okong’o Mogeni alihimiza Kanja kuhakikisha polisi wanaotumwa nyanjani wanatambulika hasa wakati wa maandamano.

“Ni kwa nini polisi wanakamata watu wakiwa wamefunika nyuso zao? Ni majambazi?” alishangaa Seneta huyo akiongeza kwamba polisi anastahili kutambuliwa na anayekamatwa ili aweze kuwasiliana ipasavyo na wakili wake.

Mawazo sawia yalikaririwa na Seneta Mteule Crystal Asige ambaye alimtaka Kanja kuheshimu maagizo ya mahakama kuhusu kutambulika kwa maafisa wa polisi nyanjani.

Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot kwa upande wake alisema kwamba sababu pekee ya kuunga mkono uteuzi wa Kanja ni imani aliyo nayo kwamba vizuizi vingi vya polisi vinayotumiwa kukusanya hongo katika kaunti ya Kericho vitaondolewa.

Enoch Wambua seneta wa Kitui alimtakia Kanja mema anapoanza kuhudumu katika wadhifa huo akimkumbusha kwamba sasa ni huduma ya taifa ya polisi na wala sio ilivyokuwa awali kabla ya kupitishwa kwa katiba mpya ya mwaka 2010.

Share This Article