Serikali imewahakikishia wananchi kwamba nchi hii ina akiba ya chakula cha kutosha kuwahimili Wakenya kwa muda mrefu.
Akitoa hakikisho hilo, Katibu katika Wizara ya Kilimo Dkt. Paul Ronoh alisema pia kuna akiba ya mazao yanayosubiri kuhifadhiwa katika Halmashauri ya Kitaifa ya Nafaka na Mazao, NCPB.
Alisema serikali iliwalenga wakulima wa mahindi katika juhudi zake za kuimarisha uzalishaji, kwa sababu mahindi ni miongoni mwa vyakula vinavyotumiwa na idadi kubwa ya Wakenya.
Ronoh aliongeza kuwa matumizi ya kila mwezi ya mahindi nchini yameongezeka kwa karibu asilimia 80 kutoka magunia milioni nne ya kilo 90 hadi magunia milioni saba ya kilo 90.
Kulingana na katibu huyo, eneo jumla kunakokuzwa mahindi pia limeongezeka kutoka ekari milioni 44 hadi ekari milioni 67.
Alisema kupitia afua mbalimbali za serikali, ikiwemo mpango wa mbolea ya ruzuku, nchi imefanikiwa kushughulikia suala la uhaba wa chakula, akiongeza kuwa mwaka huu, nchi imepata mazao ziada ya chakula.
Hata hivyo, aliwashauri wakulima kujenjga ghala za ziada kuhifadhi mazao yao, kwa sababu mavuno ya msimu huu hasa kutoka kwa sekta ya mahindi yataongezeka.
Pia aliwahakikisha wakulima kuwa serikali itawalinda kwa kununua mahindi yao kupitia NCPB kwa shilingi elfu nne kwa kila gunia la kilo 90.