Mahakama kuu imeongeza muda wa kusimamisha kikosi kazi kilichoteuliwa na Rais William Ruto kutathmini deni la taifa la Kenya.
Jaji Lawrence Mugambi alitoa maagizo hayo leo huku akiruhusu walalamishi Magare Gikenyi na Eliud Matindi kuwajuza washtakiwa wa kesi hiyo kuhusu kesi kupitia kwa gazeti ambalo linapatikana katika sehemu ya nchi.
Mahakama iliafikia uamuzi wa leo baada ya kubainika kwamba baadhi ya washtakiwa wa kesi hiyo bado hawajakabidhiwa stakabadhi za kesi.
Washtakiwa hao ni pamoja na mkaguzi mkuu wa mahesabu serikalini na walioteuliwa kuhudumu kwenye kikosi kazi hicho.
Gikenyi na Matindi walikwenda mahakamani kulalamikia uhalali wa jopo hilo wakisema kwamba Rais hana mamlaka ya kubuni jopo kama hilo na kwamba alikiuka katiba.
Waliomba pia kuzuiwa kwa jopo hilo kuanza kazi hadi kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa, agizo ambalo mahakama ilitoa Julai 9, 2024.
Walalamishi wanasema majukumu ya jopo hilo yanafanana na ya mkaguzi mkuu wa mahesabu ya matumizi ya pesa za serikali.
Julai 5, 2024, Rais William Ruto aliteua watu kadhaa kwa kikosi kazi ambacho jukumu lake kuu ni kuchunguza deni la taifa ambapo wanachama kama rais wa chama cha wanasheria nchini Faith Odhiambo walikataa uteuzi huo.
Nancy Onyango aliteuliwa mwenyekiti wa jopo hilo na Luis Franceschi akateuliwa naibu mwenyekiti.
Kesi hiyo itatajwa tena Septemba 18, 2024.