Wakenya waalikwa kutoa maoni kuhusu mswada wa utoaji wa sodo

Marion Bosire
2 Min Read

Bunge la seneti limetoa mwaliko kwa wakenya kutoa maoni yao kuhusu mswada wa utoaji wa sodo wa mwaka huu wa 2024.

Mswada huo ambao ni wa saba wa bunge la Seneti mwaka 2024, umependekezwa na Seneta mteule Gloria Orwoba na kuelekezwa kwa kamati ya bunge hilo kuhusu Leba na utunzi wa jamii Julai 3, 2024, baada ya kusomwa bungeni mara ya kwanza.

Lengo la mswada huo ni kuhakikisha kwamba serikali inatoa sodo za ubora wa hali ya juu, za kutosha na bila malipo kwa taasisi zote za umma yakiwemo magereza.

Unalenga pia kubuni kamati ya wizara mbali mbali katika kiwango cha kitaifa na kamati sawia katika kiwango cha kaunti ambazo zitajukumiwa kuhakikisha utoaji wa sodo.

Kwa sasa mswada huo uko katika kiwango cha kusomwa kwa mara ya kwanza ambapo umefikishwa katika bunge la seneti na kusomwa na karani wa bunge. Katika kiwango hicho mswada huo haujadiliwi.

Hatua inayofuata ni ya kukabidhi mswada huo kwa kamati husika ambapo utatathminiwa na kutoa fursa ya kuhusisha umma ambapo upo kwa sasa.

Maoni hayo yanaweza kuwasilishwa kwa afisi ya karani wa bunge la Seneti au kutumwa kama barua pepe kwa anwani clerk.senate@parliament.go.ke au ile ya kamati husika ambayo ni laboursocialwelfarecomm.senate@parliament.go.ke.

Jumatatu Julai 22, 2024 ndiyo siku ya mwisho ya kuwasilisha maoni hayo.

Seneta Orwoba anafahamika sana kwa kampeni ambayo amekuwa akiendesha ya kutafuta kumaliza aibu inayoambatanishwa na hedhi.

Wakati mmoja aliondolewa bungeni baada ya kuingia humo akiwa amevaa suruali ndefu ambayo ilikuwa na damu.

Share This Article