Rais Ruto: Nitafanya mabadiliko serikalini hivi karibuni

Martin Mwanje
1 Min Read

Rais William Ruto ametangaza kuwa ataifanyia mabadiliko serikali yake ya Kenya Kwanza hivi karibuni. 

Ruto amesema mabadiliko hayo yanakusudia kuboresha utendakazi wa serikali ambayo imeshutumiwa vikali na Wakenya hasa vijana wa Gen Z kwa kutotimiza ahadi ilizoahidi wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.

Tayari, Rais Ruto ametangaza hatua mbalimbali zinazokusudia kupunguza matumizi ya serikali ikiwa ni pamoja na kusitisha uteuzi wa mawaziri wasaidizi (CASs), kufutilia mbali bajeti zinazotengewa ofisi za Mke wa Rais, Mke wa Naibu Rais na Mke wa Kinara wa Mawaziri na pia kuvunjilia mbali mashirika 47 ya serikali ambayo majukumu yake yanawiana.

“Hatua hizi zitafuatwa na mabadiliko serikalini ambayo nitayatangaza hivi karibuni,” alisema Rais Ruto wakati akilihutubia taifa leo Ijumaa mchana.

“Tumedhamiria kufanya haya na mabadiliko mengine ili kuimarisha ubora, utendakazi na uwazi katika kuwahudumia Wakenya na kuhakikisha raia wanapokea thamani ya juu zaidi kutokana na rasilimali zao kutoka kwa sekta ya umma ambayo inatoa kipaumbele kwa maslahi yao.”

Katika mabadiliko hayo, Rais Ruto anatarajiwa kulifanyia mabadiliko Baraza lake la Mawaziri hasa wakati huu ambapo baadhi ya mawaziri wameshutumiwa vikali kwa kuzembea kazini.

 

 

 

 

Share This Article