Rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua leo Jumamosi, walitoa heshima zao kwa mfanyabiashara maarufu jijini Nairobi, Mzee Gerald Gikonyo Kanyuira kwa mchango wake katika sekta ya biashara na kujitolea kwake kutumikia taifa hili.
Katika taarifa iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Rais Rigathi Gachagua, wakati wa ibada ya mazishi ya mfanyabiashara Mzee Gerald Gikonyo Kanyuria, eneo la Kangema kaunti ya Murang’a, Rais William Ruto alimuomboleza Mzee Gikonyo akimtaja kuwa atakumbukwa kwa unyenyekevu wake, mwenye maadili na jasiri.
Rais Ruto alisema mzee Gikonyo alijitolea kikamilifu katika biashara, hatua iliyochochea ukuaji wa sekta ya biashara Jijini Nairobi katika enzi za ukoloni.
Kwa upande wake naibu rais Rigathi Gachagua alisema mzee Gikonyo alikuwa na ari ya kufanya biashara na alikuwa mfano bora kwa watu wengi katika sekta ya biashara kutokana na mafanikio yake.
Katika hotuba yake, naibu huyo wa Rais aliwataka viongozi kuiga mfano wa mzee Gikonyo kwa kukoma kuwadharau na kutowaheshimu wakenya, huku akiwahimiza kuwahudumia wananchi.
“Walio uongozini wanapaswa kuwaheshimu watu na kukoma kuwadharau. Wengine wanajigamba na mali waliyo nayo, huku wakisema serikali haina fedha na inakusanya ushuru kulipa madeni,” alisema Gachagua.
Mzee Gikonyo, ambaye alifariki wiki iliopita , alianza kufanya biashara mwaka wa 1930 akiwa mchuuzi jijini Nairobi.
Kwa muda wa miaka nyingi, alifanikiwa kupanua biashara yake kwa jina Rwathia Group of Companies, ambayo ni kampuni inayomiliki hoteli ya Alfa, Magomano, Timboroa, New Kinangop, kampuni ya kusambaza mvinyo ya Rwathia miongoni mwa mengine.