50 Cent ashtakiwa na mpiga picha

50 Cent ashtakiwa na mpiga picha

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki wa Marekani Curtis James Jackson III maarufu kama 50 Cent ameshtakiwa na mpiga picha kwa kile anachokitaja kuwa kugongwa na gari la mwanamuziki huyo.

Jamaa huyo anawakilishwa na wakili Gloria Rachel Allred ambaye anadai kwamba 50 Cent aliamuru mmoja wa watu waliokuwa wameabiri gari lake kugonga mteja wake.

Mpiga picha huyo alihudhuria hafla ya mwanamuziki huyo ya kutia saini nakala za kitabu chake kiitwacho ‘The Accomplice’ mnamo Septemba 11 2024, katika The Grove huko Los Angeles nchini Marekani kwa nia ya kupiga picha.

Anasema baada ya hafla hiyo, aliendesha Skuta yake kwenye barabara iliyokuwa ikitumiwa na msafara wa 50 Cent akiwa ananakili video na waliposimama kwenye eneo la makutano, mmoja wa abiria alifungua mlango kwa nguvu.

Mlango huo ulimgonga mpiga picha huyo akaanguka akajeruhiwa na Skuta yake kuharibika.

Sasa anasema imekuwa vigumu kurejelea kazi yake kutokana na majeraha aliyoyapata huku ada za hospitali zikimzidia. Anadai pia fidia ya Skuta yake.

Wakili wa 50 Cent hata hivyo anasema kwamba hawajapokea stakabadhi za kesi hiyo na iwapo watapokea wataishughulikia ipasavyo na watadai fidia ya kiwango cha juu.

Anasema hata kesi hiyo ikija, 50 Cent hakuwa dereva wa gari husika na hivyo hana kesi ya kujibu.

Share This Article