5 wafariki, 2 wajeruhiwa kwenye shambulizi Mandera

Martin Mwanje
1 Min Read

Watu watano waliuawa na wengine wawili kujeruhiwa leo Jumanne asubuhi baada ya wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab kushambulia chimbo la mawe katika eneo la Burabor, kaunti ndogo ya Mandera Masharki katika kaunti ya Mandera. 

Kamishna wa kaunti hiyo Henry Ochako amethibitisha tukio hilo.

Amesema waathiriwa walikuwa wameondoka mjini Mandera bila kusindikizwa na maafisa wa polisi kama ilivyo kawaida, kinyume cha makubaliano yaliyowekwa na wamiliki wa machimbo hayo.

Ochako aliongeza kuwa waathiriwa walishambuliwa majira ya saa 12:30 asubuhi na kusababisha vifo vya watu hao watanao.

Watu wengine walipata majeraha huku baadhi wakifanikiwa kutoroka.

“Kwa sasa tunawahoji dereva na mmiliki wa chimbo hilo kubaini ni kwa nini kundi hilo liliondoka mapema, na kwa bahati mbaya kusababisha waathiriwa kushambuliwa ,” alisema Ochako.

Familia na marafiki wa waliofariki walikusanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Mandera ili kutambua miili ya waenda zao.

Gavana wa Mandera Mohamed Adan Khalif alituma risala zake za rambirambi kufuatia kisa hicho na kuwahakikishia wakazi kwamba haki itatendeka.

Share This Article