Kindiki asema ufisadi unakwaza maendeleo nchini

Kindiki anahisi mkakati wa muda mrefu usio wa kisiasa wa kupambana na ufisadi, unaweza kuinua Kenya hadi hadhi ya dunia ya kwanza ndani ya kizazi kimoja

Marion Bosire
1 Min Read
Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki.

Naibu Rais, Profesa Kithure Kindiki, ametaja ufisadi kuwa kikwazo kikuu zaidi kwa maendeleo ya Kenya.

Katika taarifa, Profesa Kindiki alisema kuwa ufisadi umeharibu hali ya sasa na kuiba mustakabali wa nchi, akisisitiza kuwa umeenea kwa kiwango kikubwa katika asasi tatu za serikali na ngazi mbili za Serikali.

Naibu Rais Kindiki aliongeza kuwa ufisadi umechukua nafasi ya kutisha katika maisha ya kila siku ya raia, watumishi wa umma, mashirika ya kiraia, wasomi na hata taasisi za kidini.

Profesa Kindiki alisema kuwa mkakati wa muda mrefu usio wa kisiasa wa kupambana na ufisadi, hasa ule mkubwa, unaweza kuiinua Kenya hadi hadhi ya dunia ya kwanza ndani ya kizazi kimoja.

Wakati huo huo, Naibu Rais Kindiki alisema Kenya imepiga hatua katika juhudi za kurejesha uchumi, huku viashiria vya kiuchumi vya hivi karibuni vikionesha kurejea kwa utulivu wa kiuchumi kwa hatua thabiti.

Akitoa maoni kuhusu uamuzi wa Benki Kuu ya Kenya (CBK) kupunguza kiwango chake cha riba ya msingi kwa pointi 25 hadi asilimia 9.5 leo, Kindiki aliusifu uamuzi huo kama ishara madhubuti kwamba nchi inaondoka kwenye enzi ya muongo mmoja wa viwango vya juu vya riba vilivyokuwa vikiikwamisha ukuaji wa uchumi.

Share This Article