Watu 38 wamekamatwa na wengine zaidi ya 10 kujeruhiwa kwenye purukushani zilizotokana na makabiliano kati ya polisi na vijana nje ya kanisa la Jesus Winner Ministry katika barabara ya Kamiti mtaani Roysambu.
Vijana hao walipanga kuvamia kanisa hilo kupinga hatua ya Rais William Ruto, kutoa shilingi milioni 20, alipohudhuria ibada Jumapili iliyopita kugharamia ujenzi wa kanisa.
Baada ya kupata idadi kubwa ya maafisa wa polisi waliokuwa wamezingira kanisa hilo, vijana hao walirejea hadi mzunguko wa barabara ya Roysambu, na kuifunga huku wakiwasha maguruduu wakijaribu kujikusanya ndiposa waelekee kanisani.
Polisi walilazimika kuwafyatulia vitoza machozi ili kuwatawanya ambapo ni katika purukushani hizo zaidi ya 10 walijeruhiwa na wengine 38 kukamatwa.
Vijana hao walikuwa wameonekana kukerwa na hatua ya Kasisi wa kanisa hilo Edward Mwai, kupokea mchango wa shilingi milioni 20 kutoka kwa Rais na kuapa kupitia mitandaoni kuwa wangevuruga ibada ya leo.