2Face Idibia au 2Baba mwanamuziki wa Nigeria hatimaye amezungumzia utata unaohusu umiliki wa wimbo wake maarufu wa mwaka 2004 “African Queen”.
Katika mahojiano na Nedu, 2Baba alifafanua kwamba wimbo huo ambao ulimuinua na kutangaza muziki wa Nigeria nje ya nchi hiyo, uliandikwa naye pamoja na Blackface.
Blackface ambaye aliwahi kuwa kwenye bendi moja na 2Baba amekuwa akidai kwamba ni yeye pekee aliandika wimbo huo lakini 2Baba amesema walishirikiana na yeye aliandika sehemu kubwa.
“Ni ushirikiano. Niliandika sehemu kubwa, lakini tuliandika pamoja,” alisema 2Baba huku akilalamikia madai ya Blackface ya kila mara.
Msanii huyo amesema kwamba masuala ya kisheria kuhusu wimbo huo yako wazi na haelewi Blackface analenga kuafikia nini na madai yake.
“Mambo anayoyasema Blackface ni ya kuvunja moyo. Ni ya kushangaza na ni ya kuvunja moyo. Siku moja atajirudi.” alisema 2Baba kwenye mahojiano hayo.
Mwaka 2018 Blackface alichapisha hati za mahakama zilizoonyesha kwamba alikuwa amemshtaki 2Baba akidai fidia ya Naira Milioni 50, kutokana na wimbo huo.
Alidai pia kwamba aliandika wimbo mwingine ulioimbwa na 2Baba uitwao, “Let Somebody Love you”.
2Baba na Blackface walikuwa wanachama wa bendi iliyojulikana kama “Plantashun Boiz” ambapo Faze alikuwa mwanachama wa tatu. Walianzisha kundi hilo wakiwa wanafunzi wa taasisi moja ya mafunzo ya usimamizi na teknolojia huko Enugu.