Mwanamuziki nyota wa Nigeria 2Baba au 2 Face Idibia ametoa ujumbe kwa njia ya video unaolenga mashabiki wake na umma kwa jumla akisema kwamba yuko sawa kabisa.
2Baba amejitenga pia na ujumbe uliochapishwa kwenye ‘Instagram story’ na kuendelea kusisitiza kwamba yeye yuko sawa kabisa.
Katika video hiyo ambayo amechapisha kwenye akaunti yake ya mtandao wa X, mwimbaji huyo wa wimbo maarufu wa ‘African Queen’ alisema kwamba suala lake limezungumziwa sana ilhali kila familia huwa na matatizo.
“Mambo sasa yanazidi. Hali ilivyo sasa ni hatari. Ninajua kitu ambacho mashabiki wanaweza kufanya, ninajua kile ambacho watu wanaweza kufanya.” alisema msanii huyo.
Aliendelea kusema kwamba yeye yuko sawa lakini uvumi unaosambaa kulingana naye unahatarisha usalama wa mke wake Natasha na sio sawa kwa yeyote kufanya alivyofanyiwa.
“Kwa hivyo sasa ninataka kila mtu atulie. Ninataka kila mtu apoze moto. Tutatatua masuala haya. Watu huwa na matatizo kwenye nyumba zao. Haya sio mageni.” alimalizia msanii huyo.
Kwa siku kadhaa sasa 2Baba amezungumziwa sana mitandaoni ndani na nje ya Nigeria kufuatia kile kinachotajwa kuwa kushtakiwa na Natasha kwa maafisa wa polisi nchini Uingereza baada yao kuzozana.
Mashabiki wa msanii huyo wanahisi kwamba hayuko sawa katika ndoa yake mpya baada ya kuachana na mkewe wa awali Annie Macaulay.