2Baba amchumbia Natasha

Haya yanajiri wiki chache baada ya mwanamuziki huyo kutangaza utengano na mkewe Annie.

Marion Bosire
1 Min Read

Mwanamuziki anayezingirwa na utata katika masuala ya ndoa 2Baba au ukipenda 2Face Idibia amemchumbia mpenzi wake mpya kwa jina Natasha.

Video iliyochapishwa mitandaoni na Sabi Radio inaonyesha msanii huyo akimvisha pete ya uchumba Natasha Igbinedion Osawaru ambaye ni mbunge katika jimbo la Edo.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mwimbaji huyo wa wimbo maarufu ‘African Queen’ kutangaza utengano na mkewe wa miaka 13 Annie Idibia.

Alichapisha taarifa ya utengano wao na mchakato wa talaka kwenye mitandao ya kijamii na ilipotiliwa shaka akachapisha video akisema aliyoyasema ni kweli na akaunti yake haikuwa imedukuliwa.

Video hiyo sasa inathibitisha uvumi uliokuwa ukisambaa mitandaoni kuhusu uhusiano wake wa kimapenzi na mbunge huyo wa jimbo la Edo.

Alikiri mapenzi yake kwa mwanadada huyo huku akiwataka mashabiki zake wamsaidie kumshawishi ili akubali kuolewa naye.

Kabla ya hapo alikuwa amemtetea Natasha dhidi ya shutuma kwamba amemvunjia ndoa akimtaja kuwa mwanamke bomba na hakuhusika kwa vyovyote kwa yaliyotokea kati yake na Annie.

Msanii huyo ambaye jina lake halisi ni Innocent Idibia anasema kwa sasa Natasha ni kila kitu kwake huku uvumi ukienea kwamba mbunge huyo tayari ana ujauzito wa 2Baba.

Share This Article