Leo mwanamuziki tajika wa Nigeria 2Face Idibia au ukipenda 2Baba anasherehekea siku yake ya kuzaliwa anapotimiza umri wa miaka 50.
Mtunzi huyo wa wimbo maarufu ‘African Queen’ ametoa taarifa rasmi kupitia akaunti zake za mitandao ya kijamii ambapo ameangazia maisha yake, muda aliokaa kwenye muziki na mafanikio.
Katika tamko la kugusa moyo alilolitoa kwa mashabiki, marafiki, na wadau wa tasnia ya burudani kwa jumla, 2Baba alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa safari yake hadi sasa, safari ambayo anaitaja kuwa ya ‘ajabu isiyo na kifani’.
“Wengi walioanza safari hii nami hawapo tena” aliandika akiongeza kusema kwamba “na ninawaheshimu na kuenzi kumbukumbu zao ninaposherehekea wakati huu”.
Kwa unyenyekevu na heshima, nyota huyu aliyeshinda tuzo nyingi alitoa heshima kwa nguzo kuu za maisha yake, kuanzia kwa mamake, mke wake, watoto wake, hadi kwa mashabiki wake waaminifu na mfumo mzima wa burudani uliomuinua kutoka kundi la Plantashun Boiz hadi hadhi ya mwafrika mashuhuri wa bara zima.
“Kwa malkia na wafalme wangu wa Afrika, mmenibeba, mmenipa msukumo, na mmenifanya niendelee licha ya kupanda na kushuka,” 2Baba alieleza.
Ingawa mashabiki walikuwa wakisubiri kwa hamu tukio kubwa lenye nyota wengi mwezi huu, gwiji huyo alifichua kuwa sherehe rasmi ya kumbukizi ya miaka 50 na 25 imeahirishwa bali haijafutwa.
Kulingana naye, uamuzi huu umafikiwa ili aweze kufanya jambo tofauti, akiahidi tukio lisilosahaulika litakalounganisha muziki, simulizi, shukrani na upendo kwa pamoja.
“Hatua hii si yangu peke yangu,” alisisitiza. “Ni ya sisi sote tuliotembea safari hii pamoja.”
Kuanzia nyimbo zisizopitwa na wakati hadi ushirikiano uliovunja mipaka, athari ya 2Baba katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili na nusu imekuwa ya kina na pana, ikiathiri vizazi na kuinua Afrobeat hadi jukwaa la kimataifa.
2Baba alimalizia kwa ujumbe kwa mashabiki wake akisema, “Endeleeni kuwasha moto. Kilicho bora bado kinakuja. Upendo daima”.