2024 CHAN:Mbweha wa Algeria wafakamia kitoweo cha Waganda,Namboole

Algeria walianza kwa matao ya juu wakichukua uongozi kunako dakika ya 36, kupitia kwa nahodha Ayoub Ghezala, aliyeunganisha pasi ya Abderrahmane Meziane kwa kichwa.

Dismas Otuke
1 Min Read

Algeria almaarufu The Dessert Foxes, waliwadhalilisha Uganda Cranes kwa kuwapa kichapo cha mbwa msikitini baada ya kuwachachafya mabao 3-0, katika mechi ya kundi C kuwania kombe la CHAN, iliyosakatwa jana usiku kiwarani Mandela jijini Kampala, Uganda.

Algeria walianza kwa matao ya juu wakichukua uongozi kunako dakika ya 36, kupitia kwa nahodha Ayoub Ghezala, aliyeunganisha pasi ya Abderrahmane Meziane kwa kichwa.

Kipindi cha pili maji  yalizidi unga kwa Waganda, pale walipomiminiwa magoli mawili ya haraka ndani ya dakika tatu, Meziane na Soufiane Bayazid wakibusu nyavu dakika za 76 na 79 mtawalia.

Itabidi Waganda wajipange upya kwa mchuano wa pili dhidi ya Guinea Agosti 8 ,ambao hawana budi kushinda ili kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa robo fainali kwa mara ya kwanza.

Katika mechi ya kwanza uwanjani humo Guinea waliwazabua Niger bao moja bila jawabu.

Share This Article